Almasi Mswahili

Saturday, 3 September 2016

WIZARA YA ELIMU YATAKIWA KUONGEZA WATAALAMU WA AFYA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi iweke mpango
maalumu wa kuongeza wataalamu zaidi katika
sekta ya afya ndani ya nchi ili kuipunguzia Serikali
gharama za kusomesha wataalam hao nje ya nchi.
Ametoa agizo hilo Ijumaa, Septemba 2, 2016
wakati alipokagua maendeleo ya mradi wa ujenzi
wa Kampasi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na
Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na Ujenzi wa
Kituo cha Tiba cha Kimataifa cha Muhimbili katika
eneo la Mloganzila.
Amesema Serikali zilizotangulia zimefanya kazi
kubwa na nchi imefikia hatua nzuri ya kuongeza
wataalam ndani ya nchi ambao watakwenda
kutatua changamoto ya upungufu wa madaktari
bingwa kwenye hospitali za mikoa na wilaya.
Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kituo hicho cha
tiba cha kimataifa pia utawapunguzia wananchi
adha ya kutafuta fedha za kwenda kupata
matibabu nje ya nchi. Tayari upasuaji mkubwa wa
magonjwa ya moyo umeanza kufanyika nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Bw. Humphrey
Polepole awasake watu wote waliohusika na wizi wa
lita 1,000 za mafuta ya kuendeshea mitambo
katika karakana ya mkandarasi anayejenga
Kampasi hiyo.
“Wafanyakazi waache wizi. Lita 1,000 zinaondokaje
katika karakana ya mkandarasi? Hii kampuni
inayolinda kama imeshindwa kazi iondolewe na
Mkuu wa wilaya usimhurumie mwizi,” amesisitiza.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema
kukamilika kwa kampasi ya Mloganzila kutasaidia
upatikanaji wa madaktari bingwa wengi nchini
ambao watapunguza gharama za kupeleka
wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Awali, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Ephata
Kaaya alisema kukamilika kwa hospitali pamoja na
kampasi yote ya chuo kutawezesha kupunguza kwa
kiasi kikubwa uhaba wa wataalamu wa afya nchini.
Amesema hospitali hiyo itatumika kutoa huduma za
afya za kitaalam zaidi kwa magonjwa mbalimbali,
hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa
nje ya nchi kwa matibabu. Pia itapunguza
msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili.
Ujenzi wa mradi huo umegharimu Dola za
Kimarekani milioni 61, ambapo Serikali imetoa Dola
milioni 18 na Serikali ya Korea imetoa mkopo wa
Dola milioni 43. Kukamilika kwa ujenzi wa kampasi
hiyo ya Mloganzila kutawezesha chuo kuongeza
idadi ya udahili wa wanafunzi wa fani ya afya
kutoka 4,010 hadi 15,000.
Prof. Kaaya amesema mkataba wa awamu ya
kwanza ya ujenzi wa mradi huo ulisainiwa tarehe
12, Desemba, 2014 na ujenzi ulianza mwezi Julai,
2015 na unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2016.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

No comments:

Post a Comment