Wawanafunzi wa Kidato cha Sita Shule ya
Sekondari Usevya wilayani Mlele Mkoa wa Katavi,
wanadaiwa kuwashambulia kwa kuwacharaza viboko
walimu wao wawili miongoni mwao akiwemo Makamu
Mkuu wa Shule hiyo, Makonda Ng’oka
“Membele'‘ (34) ambaye ameng’olewa meno
matano kwa kipigo hicho.
Walimu hao wawili wamedai kuwa hawako tayari
kuendelea kufundisha katika shule hiyo huku
wakisisitiza kuwa ni fedheha kwao kucharazwa
viboko na wanafunzi wao wenyewe ambapo Mwalimu
Gabriel Kambona aliachwa na ngeu kichwani.
Mei mwaka huu, Ng’oka “Membele” alifikishwa
katika Mahakama ya Mkoa wa Katavi kwa tuhuma
za kumlawiti mwanafunzi wake akidaiwa kutenda
kosa hilo kati ya Novemba 2015 na Aprili mwaka
huu.
Ilisemekana kukamatwa na kufikishwa mahakamani
kwa Makamu Mkuu huyo wa shule hiyo kulifuatia
wanafunzi wa kiume wanaosoma Kidato cha Tano
sasa wako Kidato cha Sita katika shule hiyo
kumkataa na kutishia kuandamana kupinga vitendo
vyake vya kuwalawiti wanafunzi wake.
Wanafunzi hao walidai kuwa mwalimu huyo
amekuwa akiwalawiti baadhi yao ikiwa ni adhabu
mbadala wanapobainika kufanya makosa shuleni
hapo.
Hata hivyo, baada ya kutopatikana ushahidi wa
kumtia hatiani Ng’oka, Julai 27, mwaka huu
Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda
ilimwachia huru.
Mwalimu Ng’oka aliripoti kwenye kituo chake cha
kazi shuleni Usevya Agosti Mosi mwaka huu ambako
kurejea kwake shuleni hapo kunadaiwa kuamsha
hasira kwa baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita
wakidai hawapo tayari kumwona mwalimu huyo na
familia yake shuleni hapo.
Akizungumza na wanahabari jana mjini hapa,
Ng’oka alidai kuwa hayuko tayari kuendelea
kufundisha kwenye shule hiyo akihofia usalama
wake na kutokana na kipigo alichokipata cha
kushambuliwa na baadhi ya wanafunzi wake wa
kidato cha tano na cha sita wakati akiwa nyumbani
kwake na familia yake.
Akisimulia mkasa huo, alisema Agosti 12, mwaka
huu usiku alikuwa nyumbani kwake shuleni hapo
pamoja na familia yake pamoja na mwalimu
mwenzake, Gabriel Kambona aliyekuwa
amemtembelea.
“Ghafla, saa mbili usiku nikiwa maliwatoni nikioga
lilitokea kundi la wanafunzi wa kidato cha tano na
sita wakiwa na silaha za jadi kama vile fimbo,
marungu, mawe na matofali na kuanza
kuishambulia familia yangu pamoja na mwalimu
Kambona,” alieleza na kuongeza kuwa alilazimika
‘kuchomoka’ bafuni baada ya kusikia mayowe
yaliyokuwa yakipigwa na familia yake wakiomba
msaada. Alipofika sebuleni alishuhudia wanafunzi
hao wakiishambulia familia yake kwa kuwacharaza
viboko.
“Ndipo walinigeukia na kuanza kunishambulia kwa
kunipiga kwa marungu na fimbo hadi nikapoteza
fahamu nilizinduka nikiwa nimelazwa kwenye Kituo
cha Afya Usevya na kubaini kuwa nimepoteza meno
yangu matano huku nikiwa nimejeruhiwa vibaya
kichwani. Baadaye nilihamishiwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Mpanda ambako nililazwa wiki moja na
nusu kwa matibabu na sasa nimepewa rufaa niende
Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar kwa
matibabu zaidi,” alieleza.
Alidai kuwa uhasama baina yake na wanafunzi hao
umedumu kwa muda mrefu, lakini anashangaa
uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya
Mlele umeshindwa kumpangia kituo kingine cha
kazi na kuchukua hatua yoyote kwa wanafunzi hao
licha ya kupeleka majina yao kwa kuwa
anawafahamu wote waliohusika.
Mwalimu Kambona alidai kuwa hayuko tayari
kuendelea kufundisha kwenye shule hiyo kwamba
kitendo cha kupigwa na wanafunzi wake
kimemfedhehesha.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, walimu wa shule hiyo
waliketi baada ya kutokea kwa tukio hilo, na
walifikia maamuzi kuwa wanafunzi wote
waliobainika kushiriki kuwashambulia walimu wao
wasimamishwe shule akidai kuwa uongozi wa
Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele
ulipinga.
“Nimeandika barua ya kuomba uhamisho kwani nia
aibu kwangu kuendelea kufundisha wanafunzi
ambao wamenishambulia na kunitoa ngeo kichwani
….. siku hiyo ya tukio niliibiwa simu mbili za
kiganjani lakini jana nimefanikiwa kuikamata simu
moja kwa mwanafunzi wa kidato cha tano
anayeitwa , Alex Maiko Makona na tayari
amemfikisha katika Kituo cha Polisi cha Usevya,”
alidai.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa
Katavi, Gregori Mshota alisema tayari chama
chake kimeanza kuwasiliana na uongozi wa
Halmashauri ya Mpimbwe na uongozi wa Wilaya ya
Mlele ili kuhakikisha mwalimu huyo anakuwa
salama.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Katavi, Ernest Hinju
alidai kuwa suala hilo lipo ofisini kwake na
wameanza kulitafutia ufumbuzi. “Jambo hili
linahitaji ushirikishwaji wa vyombo mbalimbali
ikiwemo Bodi ya Shule ya Sekondari ya Usevya,”
alieleza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa katika
ziara mkoani Katavi mwezi uliopita, mke wa
mwalimu Ng’oka alitinga kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika kijijini Maji Moto akiwa na
bango lenye malalamiko ya kutishiwa usalama wa
maisha wa familia yake, na Waziri Mkuu alimwagiza
Kamanda wa Polisi wa Mkoa kushughulikia
malalamiko hayo.
Welcome to our blog,this blog is deals with the all news about education and it allow teachers and other education dealers to discuss different things.
Tuesday, 13 September 2016
WANAFUNZI WAWATANDIKA FIMBO WALIMU WAO
Labels:
Mswahili
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment