Almasi Mswahili

Tuesday, 13 September 2016

AJIRA MPYA ZANUKIA

Serikali imeanza kupanga walimu wa sayansi moja
kwa moja katika shule badala ya Halmashauri kama
ilivyokuwa awali ili kuleta uwiano sawa wa walimu
katika shule mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (TAMISEMI) Suleman Jaffo alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Muleba Prof. Anna
Tibaijuka lililohusu mkakati wa Serikali katika
kukabiliana na tatizo la upungufu wa walimu.
Naibu Waziri Jaffo amesema kuwa Serikali
imeandaa mkakati wa kuwaajiri wahitimu wa
shahada za sayansi ambazo siyo za ualimu baada ya
kuwapa mafunzo ya muda mfupi kuhusu mbinu za
ufundishaji na maadili ya ualimu ili kukabiliana na
changamoto ya walimu wa sayansi nchini.
Naibu Waziri Jaffo amesema kuwa tayari kibali
kimeombwa katika Ofisi ya Rais Utumishi kwa ajili
ya utekelezaji huo, ambapo Serikali imepanga
kuajiri walimu wastaafu wenye uwezo wa
kufundisha waliokuwa wanafundisha masomo ya
sayansi kwa mkataba ili kupunguza pengo lililopo.
Aidha, Naibu Waziri Jaffo amebainisha kuwa
Serikali inafanya tathimini ya mahitaji ya walimu
wa masomo ya sanaa kwa kila Halmashauri ili
kubaini maeneo yenye ziada na yenye upungufu ili
kusawazisha.
“Mpango wa Serikali uliopo ni kuwahamasisha
walimu wa ziada wa masomo ya sanaa kwenda
kufundisha katika shule za msingi ndani ya
Halmashauri husika, ambapo kabla ya kuanza
utekelezaji wa mabadiliko haya Serikali itatoa
waraka maalumu kwenda katika Halmashauri zote
nchini ” amefafanua Naibu Waziri huyo.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa mafunzo ya
walimu Mhe. Jaffo amesema kuwa Halmashauri
moja haiwezi kuwa na mfumo wa peke yake wa
kuandaa walimu hali ambayo iltakuwa ni vigumu
kuthibiti ubora wa mafunzo hayo kwa walimu.
Hata hivyo amesema kuwa Serikali itaendelea
kuongeza udahili wa walimu wa sayansi katika vyuo
vya ualimu kadri watakavyojitokeza ili kukidhi
mahitaji yaliyopo

No comments:

Post a Comment