Almasi Mswahili

Sunday, 9 October 2016

FAGIA FAGIA WIZARA YA ELIMU YAENDELEA

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi imezifuta shule nyingine za awali na msingi
nchini ambazo hazijasajiliwa zaidi ya 10 kuanzia
Desemba mwaka jana. Aidha, shule tano kati ya 40
zilizokuwa zimefutiwa usajili zimekamilisha taratibu
na kurejeshewa usajili wake.
Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Shule katika
wizara hiyo, Khadija Mcheka amesema mpaka sasa
bado wanaendelea na ukaguzi kubaini shule ambazo
hazijasajiliwa.
Alizitaja shule ambazo zimefutwa kwa kutosajiliwa
kuwa ni Mwandai Junior Academy, shule ya msingi
DACETE, shule za msingi Malaika na Fares Kisingo
(FK) za wilaya ya Kinondoni. Nyingine ni shule ya
msingi The Unity, shule ya sekondari Jotac iliyopo
eneo la Kipunguni, Verena iliyopo eneo la Pugu
zote wilaya ya Ilala, Exodus iliyopo Kigamboni na
Havard Junior ya wilaya ya Temeke.
Alisema shule nyingine zilizofutwa kabisa ni shule
ya sekondari ya Kahe ambayo imefutwa kutokana
na wamiliki kushindwa kuiendesha na pia majengo
yake yamebadilishiwa matumizi.
Alisema shule nyingine za Deogrolius International
School iliyopo Kitunda, Desinity na Almustakim
zote za jijini Dar es Salaam nazo zimefutiwa
usajili. Alisema awali yalitolewa majina ya wamiliki.
Mcheka alisema pia shule mbili hazitakiwi kuwa za
bweni ambazo ni Heritage iliyopo Banana Ukonga
na Hellens iliyopo Kinondoni.
Akizungumzia shule zilizorejeshewa usajili, alisema
ni Gisera, Rose Land, Conerstone na Grace za
jijini Dar es Salaam na Must Lead na Qunu zilizopo
mkoani Pwani huku shule ya Fountain Gate
ikifutiwa usajili wa kuendesha shughuli za bweni.
Akifafanua kuhusu shule ya Coner Stone alisema
baada ya ukaguzi na kufutiwa usajili kuanzia mwezi
Julai zipo shule ambazo zilikamilisha utaratibu na
kurejeshewa usajili, na kwamba hakuna shule
iliyoelezwa kufutiwa usajili kwa uongo.
“Kuhusu shule zinazolalamika kutangazwa kimakosa
si kweli isipokuwa jambo lililofanyika baada ya
kuwapelekea barua kuwataka kutawanya wanafunzi
baada ya kufutiwa usajili walikamilisha utaratibu
ndipo wakasajiliwa,“ alisisitiza.
Alisema ukaguzi huo wa shule unaendelea katika
mikoa yote nchini kwa kuwatumia wakaguzi wa
Kanda na watakaobainika watafutwa mpaka
watakapokidhi vigezo vinavyotakiwa.
Hivi karibuni Mcheka alisema kuanzia Julai hadi
Desemba mwaka jana, waligundua kuwepo kwa
shule 35 zisizosajiliwa na kuzifuta na baadaye
walizifungia shule nyingine 12.
Mcheka alisema shule zinaweza kufutwa kwa
sababu mbili zikiwamo zilizosajiliwa, lakini zikakiuka
vigezo ambapo zikitimiza vigezo zinaweza kuomba
upya usajili na kupewa.
“Lakini aina ya pili ni zile ambazo hazijasajiliwa na
zinaendeshwa kinyume cha sheria ambazo nazo
zikifuata taratibu zikatimiza vigezo zinaweza
kupewa usajili,” alifafanua Kaimu Mkurugenzi huyo
wa Usajili wa Shule.
Alisema katika kipindi hicho mpaka Agosti mwaka
huu baada ya tangazo la kuwataka kusajiliwa shule
za awali nne, zile za awali na msingi 105 na
sekondari 19, walifika wizarani kwa ajili ya kupata
taratibu za usajili ambapo zipo zilizosajiliwa na
nyingine kupewa vibali.
Alisema katika usajili, wapo waliokidhi viwango na
wengine walipatiwa maelekezo na kupatiwa vibali
vya kutumia majengo yaliyopo huku wengine
wakipewa vibali vya kujenga majengo ya shule
kabla ya kupata usajili.
Alisema kwa shule walizozifungia, waliwaandikia
barua za kuwafungia na kuwataka kuhakikisha
wanawatawanya wanafunzi katika shule
zilizosajiliwa kwa gharama zao bila kuwaathiri
wanafunzi.
Alitaja shule zilizofungiwa kwa kuendesha shughuli
zake bila usajili kuwa ni shule ya awali na msingi
Must Lead ya mkoa wa Pwani, kwa upande wa
mkoa wa Dar es Salaam ni Brainstorm, Pax,
Lassana, Grace, Rose Land, Julius Raymod, St
Thomas, Mary Mother of Mercy, Noble Sinkonde,
Immaculate Heart of Mary, St Columba, Corner
Stone, Dancraig, Mwalimu Edward Kalunga, Edson
Mwidunda, Gisela, Kingstar, St Columba, Bilal
Muslim, Thado, Hocet , Elishadai, Lawrance
Citizen, Comrade, Dar Elite Preparatory, Golden
Hill Academy na Hekima.
Nyingine ni Pwani Islamic, St Kizito na Rwazi
Encysloped za Kagera, Dancraig na Qunu za Pwani,
Hellen’s ya Njombe, Joseph ya Arusha, Samandito
na Maguzu za Geita. Alizitaja shule za sekondari
zilizofungiwa kwa sababu hiyo kuwa ni Hananasif,
Elu, Hocet, Safina za Dar es Salaam na Namnyaki
ya Iringa.

No comments:

Post a Comment