Almasi Mswahili

Sunday, 9 October 2016

EWE MTUMISHI JIANDAE KWA HILI

Hatua ya Baraza la Mitihani nchini (Necta) kutoa
ratiba ya kufanya uhakiki wa vyeti vya kidato cha
nne, sita na ualimu kwa watumishi wote wa umma
sasa ni wazi imezidi kupandisha joto kwa vigogo na
watumishi mbalimbali ambao hawana sifa za kielimu
kushika nafasi walizo nazo.
Katika taarifa yake ya sasa Baraza la Mitihani
nchini, limetangaza kuwafuata katika maeneo yao
ya kazi watumishi wote walioko katika mamlaka za
mikoa, halmashauri na manispaa kwa ajili ya
kufanya uhakiki wa vyeti vyao hivyo vya kitaaluma.
Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na Edga Kasuga
kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo
kwenda kwa Makatibu tawala wa Mikoa, uhakiki
utafanyika katika ofisi za Makatibu Tawala wa
mikoa kuanzia Oktoba 10 hadi 14 mwaka huu,
ingawa ratiba nyingine ya uhakiki imeonyesha zoezi
hilo litafikia tamati Novemba 7 mwaka huu.
“Ili kufanikisha zoezi hilo Baraza limetaka kupata
orodha (nakala- laini ya soft copy) ya watumishi
wote wa umma waliopo katika Mkoa, Halmashauri
na Manispaa.
“Nakala za vyeti vya kidato cha nne, cha sita na
ualimu vya watumishi wote walioandikishwa na
chumba cha kufanyia uhakiki,” inaeleza taarifa
hiyo ya Baraza la Mitihani.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la
Mitihani, uhakiki huo utafanywa katika makundi
matano katika mikoa tofauti tofauti.
Oktoba 10, mwaka huu kundi la kwanza litafanya
uhakiki katika Mkoa wa Mtwara, kundi la pili
Singida, kundi la tatu Rukwa, kundi la nne Katavi
na kundi la tano litakuwa Geita.
Oktoba 17 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa
Lindi, la pili Manyara la tatu Songwe, la nne
Kigoma na la tano litakuwa Mwanza.
Oktoba 24 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa
Morogoro, la pili Arusha, la tatu Mbeya, la nne
Tabora na la tano Mara.
Oktoba 31 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa
Pwani, la pili Kilimanjaro, tatu Ruvuma, la nne
Shinyanga na la tano Simiyu.
Novemba 7 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa
Dar es Salaam, la pili Tanga, la tatu Njombe, la
nne Dodoma na la tano Iringa.

No comments:

Post a Comment