Almasi Mswahili

Thursday, 20 October 2016

TSNP WAJIPANGA KUMFUATA WAZIRI WA ELIMU

Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania
( TSNP) umepanga kuunda kamati ya viongozi wa
serikali za vyuo vikuu ili kukutana kwa dharura na
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Joyce
Ndalichako.
Pia imepanga kuandaa tamko la kupinga tamko la
mabadiliko ya vigezo vitakavyozingatiwa katika
utoaji mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu,
lililotolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Elimu
Mhandisi Stella Manyanya.
Mtandao huo umedai kuwa, mabadiliko hayo ya
vigezo yamesababisha wanafunzi wengi kukosa
mikopo huku baadhi yao kupunguziwa fedha za
kujikimu.
Mkurugenzi wa Haki za Wanafunzi TSNP, Venancy
Shitindi jana alisema kuwa TSNP kwa sasa
inakusanya taarifa za changamoto zinazo wakabili
wanafunzi waliokosa mikopo ili kuandaa tamko la
kupinga mabadiliko hayo, litakalo pelekwa katika
Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu.
“Tumepanga kutengeneza kamati ndogo ya viongozi
kwa ajili ya kukutana kwa dharura na waziri mwenye
dhamana ya elimu ili kutoa malalamiko ya wanafunzi
juu ya vigezo vipya vilivyotolewa na wizara yake, pia
tunakusanya taarifa na kuandaa tamko
tutakalolisambaza katika ofisi ya rais, wizara ya
elimu na ofisi ya waziri mkuu,” alisema.
Alidai kuwa, mtandao huo umefanya utafiti wa
vigezo vipya vilivyotajwa na kubaini kuwa
haviendani na sera ya elimu ya mwaka 2014, wala
ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na
mpango mkakati wa kitaifa wa maendeleo kama
alivyosema Mhandisi Manyanya katika taarifa yake
aliyoitoa kwa vyombo vya habari.
“Baada ya kusoma taarifa ya Naibu Waziri Manyanya
tulikwenda kuangalia sera ya elimu ya mwaka 2014,
tukakuta hakuna sehemu iliyoainisha kundi
linalostahili kupata mkopo bali imeeleza elimu
itolewe bure na mikopo itolewe kwa kila
mwanafunzi. Na kwamba elimu imepewa kipaumbele
cha kuleta maendeleo katika nyanja zote haijasema
kwa wanaosomea masomo ya sayansi pekee,”
alisema na kuongeza.
“Hata mpango wa maendeleo wa miaka 5 yaani
2025, unaeleza kuwa Tanzania inatakiwa kuwa na
uchumi wa kati na kwamba imetoa kipaumbele elimu
kutolewa bure kwa nyanja zote ili wapatikane
wataalamu wa fani mbalimbali na wa kutosha.”
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Mhandisi
Manyanya ilisema kuwa serikali kupitia Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, huandaa sifa
na vigezo vya utoaji Mikopo kila mwaka ili
kuendana na malengo na matarajio yaliyopo katika
mipango na mikakati ya kitaifa kama ilivyoainishwa
katika Dira ya Taifa 2025.
Na kwamba Serikali imetoa vipaumbele katika utoaji
mikopo kwa wanafunzi wa mafunzo ya Fani za
Sayansi za Tiba na Afya,Ualimu wa Sayansi na
Hisabati, Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo,
Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi Asilia na Mabadiliko
ya Tabianchi, Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na
Miundombinu.

ⓒMswahili

No comments:

Post a Comment