Almasi Mswahili

Thursday, 20 October 2016

MIKOPO KWA WANAOSOMA VYUO VIKUU BADO NI KIZUNGUMKUTI.

Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) imetuliza hasira za wanafunzi wa vyuo
vikuu kwa kurejesha posho ya chakula na malazi
ya Sh8,500 kwa kila mmoja na kwamba tofauti
baina yao itakuwa viwango vya ada.
Ufafanuzi huu uliotolewa jana usiku na Waziri wa
Elimu, Sayansi , Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi
Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumza
katika mahojiano maalimu na kituo cha runinga
cha Taifa -TBC utakuwa faraja kwa wanafunzi
ambao chini ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) walipanga
kushinikiza walipwe posho ya Sh8,500 kwa siku
kama ilivyokuwa awali.
Hatua ya wanafunzi kujenga umoja ili kushinikiza
haki katika posho ilitokana na baadhi yao
kuingiziwa kati ya Sh40,000 na 70,000 badala ya
Sh 510,000, hali ambayo ilizua sintofahamu.
Ndalichako alisema tofauti ya malipo itakuwa
katika ada na siyo posho, “Vigezo vya mikopo
vimebadilika, kila mwanafunzi atapata fedha tofauti
lakini tumefanya marekebisho kwenye posho ya
chakula ambayo kila mwanafunzi atalipwa Sh8,500
kama awali.”
Kwa mujibu wa utaratibu wa Bodi hiyo, malipo
hayo ya chakula na malazi hutolewa kila baada ya
miezi miwili.
Mapema jana, Daruso iliwataka wanafunzi wa chuo
hicho kutotia saini fomu za fedha za mikopo yao
mpaka itakapowapa ruhusa ya kufanya hivyo.
Rais wa Daruso, Erasmi Leon alisema hayo jana
wakati akizungumza na wanafunzi wenzake kuhusu
kusudio la kwenda HESLB kwa ajili ya kutafuta
haki yao ya msingi.
“Ninachowasihi tuwe pamoja. Tuwe wamoja na
twende pamoja. Tutakwenda wawakilishi kutafuta
nafasi kwa amani waweze kusikia tuna hoja gani
lakini tukinyimwa hii nafasi tutaenda kuitafuta
tukiwa wengi,” alisema na kuongeza:
“Tuwe watulivu kwa sasa tutakapowahitaji muda
na wakati wowote kwa lolote tushirikiane ili twende
pamoja tumalize pamoja tuhakikishe tunapata
Sh8,500 kwa kila mwanafunzi kwa chakula na
malazi,” alisema.
Kuhusu suala hilo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM) ulisema wajibu wake ni
kupokea na kusambaza majina na taarifa kutoka
Bodi kwa wanafunzi.
Akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi waliofika ofisini
kwake kujua hatima yao na waliopata mikopo
kuchukua fomu za kutia saini, Ofisa Mikopo wa
UDSM, Lugano Mwakyusa alisema wenye jukumu
la kujua walio na sifa ya kupata mikopo ni Bodi ya
Mikopo.
“Tunaendelea kupokea majina kutoka bodi. Tayari
hapa kuna majina 949 yameshatoka, wengine tuzidi
kusubiri na wale mwaka wa pili na tatu ambao
walikuwa na mitihani ya marudio taarifa zao
zitapelekwa bodi,” Mwakyusa aliwaambia
wanafunzi waliokuwa wamejaa ofisini kwake.
Kulikuwa na hali ya sintofahamu chuoni hapo jana
baada ya wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza
kuonekana wakiwa wameshika bahasha za kaki
zilizokuwa na fomu za usajili wanazotakiwa kujaza
huku wakihangaika kutokana na kutojua kiasi cha
mkopo.
Juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, AbdulRazaq
Badru alieleza kwamba ingawa wanafunzi 88,000
waliomba mikopo kutoka HESLB, uwezo wa bodi
hiyo ni kutoa kwa wanafunzi 21,500 pekee sawa
na asilimia 24 na waliokuwa wameshapatiwa
walikuwa 11,000 sawa na asilimia 12.
Takwimu hizi zinaonyesha zaidi ya robo tatu ya
wanafunzi wanaohitaji mikopo watakosa kutokana
na uwezo mdogo wa kifedha.

TSNP WAJIPANGA KUMFUATA WAZIRI WA ELIMU

Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania
( TSNP) umepanga kuunda kamati ya viongozi wa
serikali za vyuo vikuu ili kukutana kwa dharura na
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Joyce
Ndalichako.
Pia imepanga kuandaa tamko la kupinga tamko la
mabadiliko ya vigezo vitakavyozingatiwa katika
utoaji mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu,
lililotolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Elimu
Mhandisi Stella Manyanya.
Mtandao huo umedai kuwa, mabadiliko hayo ya
vigezo yamesababisha wanafunzi wengi kukosa
mikopo huku baadhi yao kupunguziwa fedha za
kujikimu.
Mkurugenzi wa Haki za Wanafunzi TSNP, Venancy
Shitindi jana alisema kuwa TSNP kwa sasa
inakusanya taarifa za changamoto zinazo wakabili
wanafunzi waliokosa mikopo ili kuandaa tamko la
kupinga mabadiliko hayo, litakalo pelekwa katika
Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu.
“Tumepanga kutengeneza kamati ndogo ya viongozi
kwa ajili ya kukutana kwa dharura na waziri mwenye
dhamana ya elimu ili kutoa malalamiko ya wanafunzi
juu ya vigezo vipya vilivyotolewa na wizara yake, pia
tunakusanya taarifa na kuandaa tamko
tutakalolisambaza katika ofisi ya rais, wizara ya
elimu na ofisi ya waziri mkuu,” alisema.
Alidai kuwa, mtandao huo umefanya utafiti wa
vigezo vipya vilivyotajwa na kubaini kuwa
haviendani na sera ya elimu ya mwaka 2014, wala
ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na
mpango mkakati wa kitaifa wa maendeleo kama
alivyosema Mhandisi Manyanya katika taarifa yake
aliyoitoa kwa vyombo vya habari.
“Baada ya kusoma taarifa ya Naibu Waziri Manyanya
tulikwenda kuangalia sera ya elimu ya mwaka 2014,
tukakuta hakuna sehemu iliyoainisha kundi
linalostahili kupata mkopo bali imeeleza elimu
itolewe bure na mikopo itolewe kwa kila
mwanafunzi. Na kwamba elimu imepewa kipaumbele
cha kuleta maendeleo katika nyanja zote haijasema
kwa wanaosomea masomo ya sayansi pekee,”
alisema na kuongeza.
“Hata mpango wa maendeleo wa miaka 5 yaani
2025, unaeleza kuwa Tanzania inatakiwa kuwa na
uchumi wa kati na kwamba imetoa kipaumbele elimu
kutolewa bure kwa nyanja zote ili wapatikane
wataalamu wa fani mbalimbali na wa kutosha.”
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Mhandisi
Manyanya ilisema kuwa serikali kupitia Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, huandaa sifa
na vigezo vya utoaji Mikopo kila mwaka ili
kuendana na malengo na matarajio yaliyopo katika
mipango na mikakati ya kitaifa kama ilivyoainishwa
katika Dira ya Taifa 2025.
Na kwamba Serikali imetoa vipaumbele katika utoaji
mikopo kwa wanafunzi wa mafunzo ya Fani za
Sayansi za Tiba na Afya,Ualimu wa Sayansi na
Hisabati, Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo,
Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi Asilia na Mabadiliko
ya Tabianchi, Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na
Miundombinu.

ⓒMswahili

Wednesday, 12 October 2016

SAKATA LA MBEYA DAY RC KAYAONGEA HAYA

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala
amesema kuwa wanafunzi wa ualimu na walimu
waliohusika na tukio la kumpiga mwanafunzi
katika Shule ya Sekondari ya Kutwa Mbeya tayari
wanaendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi kufuatia
tukio hilo.
Licha ya kuwa tukio lile halikuwa adhabu sahihi
kwa mwanafunzi, Mkuu wa Mkoa amewataka
wazazi kujijengea tabia ya kuwafuatilia watoto wao
kwani ameleeza kuwa nidhamu ya wanafunzi wa
shule hiyo ni mbovu sana hasa kwa wanafunzi wa
kidato cha tatu na cha nne.
Mkuu wa mkoa ameeleza kuwa, kuna wakati
darasa lenye wanafunzi 50, mwalimu anafundisha
wanafunzi 10 pekee wengine wakiwa hawamo
darasani na mara kadhaa wanapishana na
mwalimu wakati wanaingia wao wanatoka.
Wanafunzi wengine wamediriki hata kukunjiana
ngumi na walimu, hivyo baadhi ya walimu ili
kuepusha shari wamewaacha wafanye waoonavyo
vyema.
Mkuu wa mkoa amesema kuwa wataendelea
kufanya uchunguzi kuwabaini wanafunzi wakarofi
zaidi na adhabu stakihi zitachukua hatua mara
moja ili kuweza kurejesha nidhamu katika shule
mkoani humo.
***********************************
Mswahili

Sunday, 9 October 2016

EWE MTUMISHI JIANDAE KWA HILI

Hatua ya Baraza la Mitihani nchini (Necta) kutoa
ratiba ya kufanya uhakiki wa vyeti vya kidato cha
nne, sita na ualimu kwa watumishi wote wa umma
sasa ni wazi imezidi kupandisha joto kwa vigogo na
watumishi mbalimbali ambao hawana sifa za kielimu
kushika nafasi walizo nazo.
Katika taarifa yake ya sasa Baraza la Mitihani
nchini, limetangaza kuwafuata katika maeneo yao
ya kazi watumishi wote walioko katika mamlaka za
mikoa, halmashauri na manispaa kwa ajili ya
kufanya uhakiki wa vyeti vyao hivyo vya kitaaluma.
Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na Edga Kasuga
kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo
kwenda kwa Makatibu tawala wa Mikoa, uhakiki
utafanyika katika ofisi za Makatibu Tawala wa
mikoa kuanzia Oktoba 10 hadi 14 mwaka huu,
ingawa ratiba nyingine ya uhakiki imeonyesha zoezi
hilo litafikia tamati Novemba 7 mwaka huu.
“Ili kufanikisha zoezi hilo Baraza limetaka kupata
orodha (nakala- laini ya soft copy) ya watumishi
wote wa umma waliopo katika Mkoa, Halmashauri
na Manispaa.
“Nakala za vyeti vya kidato cha nne, cha sita na
ualimu vya watumishi wote walioandikishwa na
chumba cha kufanyia uhakiki,” inaeleza taarifa
hiyo ya Baraza la Mitihani.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la
Mitihani, uhakiki huo utafanywa katika makundi
matano katika mikoa tofauti tofauti.
Oktoba 10, mwaka huu kundi la kwanza litafanya
uhakiki katika Mkoa wa Mtwara, kundi la pili
Singida, kundi la tatu Rukwa, kundi la nne Katavi
na kundi la tano litakuwa Geita.
Oktoba 17 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa
Lindi, la pili Manyara la tatu Songwe, la nne
Kigoma na la tano litakuwa Mwanza.
Oktoba 24 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa
Morogoro, la pili Arusha, la tatu Mbeya, la nne
Tabora na la tano Mara.
Oktoba 31 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa
Pwani, la pili Kilimanjaro, tatu Ruvuma, la nne
Shinyanga na la tano Simiyu.
Novemba 7 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa
Dar es Salaam, la pili Tanga, la tatu Njombe, la
nne Dodoma na la tano Iringa.

FAGIA FAGIA WIZARA YA ELIMU YAENDELEA

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi imezifuta shule nyingine za awali na msingi
nchini ambazo hazijasajiliwa zaidi ya 10 kuanzia
Desemba mwaka jana. Aidha, shule tano kati ya 40
zilizokuwa zimefutiwa usajili zimekamilisha taratibu
na kurejeshewa usajili wake.
Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Shule katika
wizara hiyo, Khadija Mcheka amesema mpaka sasa
bado wanaendelea na ukaguzi kubaini shule ambazo
hazijasajiliwa.
Alizitaja shule ambazo zimefutwa kwa kutosajiliwa
kuwa ni Mwandai Junior Academy, shule ya msingi
DACETE, shule za msingi Malaika na Fares Kisingo
(FK) za wilaya ya Kinondoni. Nyingine ni shule ya
msingi The Unity, shule ya sekondari Jotac iliyopo
eneo la Kipunguni, Verena iliyopo eneo la Pugu
zote wilaya ya Ilala, Exodus iliyopo Kigamboni na
Havard Junior ya wilaya ya Temeke.
Alisema shule nyingine zilizofutwa kabisa ni shule
ya sekondari ya Kahe ambayo imefutwa kutokana
na wamiliki kushindwa kuiendesha na pia majengo
yake yamebadilishiwa matumizi.
Alisema shule nyingine za Deogrolius International
School iliyopo Kitunda, Desinity na Almustakim
zote za jijini Dar es Salaam nazo zimefutiwa
usajili. Alisema awali yalitolewa majina ya wamiliki.
Mcheka alisema pia shule mbili hazitakiwi kuwa za
bweni ambazo ni Heritage iliyopo Banana Ukonga
na Hellens iliyopo Kinondoni.
Akizungumzia shule zilizorejeshewa usajili, alisema
ni Gisera, Rose Land, Conerstone na Grace za
jijini Dar es Salaam na Must Lead na Qunu zilizopo
mkoani Pwani huku shule ya Fountain Gate
ikifutiwa usajili wa kuendesha shughuli za bweni.
Akifafanua kuhusu shule ya Coner Stone alisema
baada ya ukaguzi na kufutiwa usajili kuanzia mwezi
Julai zipo shule ambazo zilikamilisha utaratibu na
kurejeshewa usajili, na kwamba hakuna shule
iliyoelezwa kufutiwa usajili kwa uongo.
“Kuhusu shule zinazolalamika kutangazwa kimakosa
si kweli isipokuwa jambo lililofanyika baada ya
kuwapelekea barua kuwataka kutawanya wanafunzi
baada ya kufutiwa usajili walikamilisha utaratibu
ndipo wakasajiliwa,“ alisisitiza.
Alisema ukaguzi huo wa shule unaendelea katika
mikoa yote nchini kwa kuwatumia wakaguzi wa
Kanda na watakaobainika watafutwa mpaka
watakapokidhi vigezo vinavyotakiwa.
Hivi karibuni Mcheka alisema kuanzia Julai hadi
Desemba mwaka jana, waligundua kuwepo kwa
shule 35 zisizosajiliwa na kuzifuta na baadaye
walizifungia shule nyingine 12.
Mcheka alisema shule zinaweza kufutwa kwa
sababu mbili zikiwamo zilizosajiliwa, lakini zikakiuka
vigezo ambapo zikitimiza vigezo zinaweza kuomba
upya usajili na kupewa.
“Lakini aina ya pili ni zile ambazo hazijasajiliwa na
zinaendeshwa kinyume cha sheria ambazo nazo
zikifuata taratibu zikatimiza vigezo zinaweza
kupewa usajili,” alifafanua Kaimu Mkurugenzi huyo
wa Usajili wa Shule.
Alisema katika kipindi hicho mpaka Agosti mwaka
huu baada ya tangazo la kuwataka kusajiliwa shule
za awali nne, zile za awali na msingi 105 na
sekondari 19, walifika wizarani kwa ajili ya kupata
taratibu za usajili ambapo zipo zilizosajiliwa na
nyingine kupewa vibali.
Alisema katika usajili, wapo waliokidhi viwango na
wengine walipatiwa maelekezo na kupatiwa vibali
vya kutumia majengo yaliyopo huku wengine
wakipewa vibali vya kujenga majengo ya shule
kabla ya kupata usajili.
Alisema kwa shule walizozifungia, waliwaandikia
barua za kuwafungia na kuwataka kuhakikisha
wanawatawanya wanafunzi katika shule
zilizosajiliwa kwa gharama zao bila kuwaathiri
wanafunzi.
Alitaja shule zilizofungiwa kwa kuendesha shughuli
zake bila usajili kuwa ni shule ya awali na msingi
Must Lead ya mkoa wa Pwani, kwa upande wa
mkoa wa Dar es Salaam ni Brainstorm, Pax,
Lassana, Grace, Rose Land, Julius Raymod, St
Thomas, Mary Mother of Mercy, Noble Sinkonde,
Immaculate Heart of Mary, St Columba, Corner
Stone, Dancraig, Mwalimu Edward Kalunga, Edson
Mwidunda, Gisela, Kingstar, St Columba, Bilal
Muslim, Thado, Hocet , Elishadai, Lawrance
Citizen, Comrade, Dar Elite Preparatory, Golden
Hill Academy na Hekima.
Nyingine ni Pwani Islamic, St Kizito na Rwazi
Encysloped za Kagera, Dancraig na Qunu za Pwani,
Hellen’s ya Njombe, Joseph ya Arusha, Samandito
na Maguzu za Geita. Alizitaja shule za sekondari
zilizofungiwa kwa sababu hiyo kuwa ni Hananasif,
Elu, Hocet, Safina za Dar es Salaam na Namnyaki
ya Iringa.